Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
imesema, inatarajia kuzima mitambo ya kurusha matangazo ya televisheni
ya mfumo wa analojia katika Mji wa Moshi na Jiji la Arusha Machi 31
mwaka huu.
Kuzimwa kwa maeneo hayo kunafikisha jumla ya mikoa
sita ambayo ni Dar es Salaam, Tanga, Dodoma na Mwanza ambayo tayari
inapokea matangazo ya televisheni kwa njia ya dijitali na kubaki Mkoa wa
Mbeya utakaozimwa Aprili 30, mwaka huu.
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Inocent Mungi
akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania cha Shirika la Utangazaji
TBC1 juzi, aliwataka wadau kushirikiana na TCRA ili kuondoa changamoto
zilizopo zinazotokana na mfumo huo.
“Bado tutaendelea kutoa elimu na tumebakiza miezi
18 katika kuhamia mfumo wa dijitali kwa dunia nzima, hivyo ni lazima
kujidhatiti”alisema Mungi.
Meneja huyu akifafanua kuhusu baadhi ya wamiliki
wa vituo vya televisheni ambao wamekuwa wakitoa taarifa za kutaka
kujitoa kurusha matangazo kutokana na kuelemewa na gharama alisema
hawana ukweli wowote.
“Wamiliki wote wa vituo wakati wakisaini leseni za
kurusha matangazo walikubali kuhimili gharama, hivyo kusema hawana
uwezo wanakuwa wanatofautiana na leseni zao” alisema Mungi.
Kauli hiyo ya Mungi inafuatia Kauli ambazo
zimekuwa zikitolewa na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya habari (Moat)
kusitisha kurusha matangazo.
SOURCE: Mwananchi